Quantcast
Channel: Magazeti ya Tanzania - Tanzania Newspapers | Magazetini
Viewing all articles
Browse latest Browse all 132783

Hammer Q: Sijatusua, bado naudai muziki

$
0
0
NA JEREMIA ERNEST ZIPO nyingi ila ‘Pembe la Ng’ombe’ akiwa na Bendi ya Dar Modern Taarab, ndiyo ngoma iliyothibitisha kuwa si tu Bongo Fleva, hata muziki huo wa mwambao anauweza. Huyo si mwingine, ni Hussein Mohamed ‘Hammer Q’, ambaye alitamba zaidi katika miaka ya 2000, akitumia ngoma ya ‘Lady’ kujitambulisha Bongo Fleva. Kipindi hicho jamaa alikuwa chini ya lebo ya Simoti Vibe ambayo kwa sasa mashabiki wa burudani nchini wanaifahamu kama Nyumba ya Vipaji (House of Talent – THT). Akimbia shule kisa muziki Msanii huyo ni mzaliwa wa Nungwi, Zanzibar, akipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Gububu. Baadaye, alijiunga kidato cha kwanza hadi cha tatu katika Shule ya Sekondari Tumekuja. “Niligundua kipaji changu cha kuimba nikiwa sekondari. Wakati huo nilikuwa nasoma huku nafanya kazi ya kunyoa watu nywele. Hivyo, saluni ilikuwa sehemu kubwa ya kufanyia mazoezi. Anasema baadaye aliamua kuacha shule na kuhamia Dar es Salaam kutafuta njia za kutoka katika muziki. “Nilikaa takribani miaka miwili bila ya mafanikio, ndipo niliposikia kuna mashindano ya ‘Zanzibar Talent Show’ ambayo yalikuwa yanaratibiwa na marehemu Ruge Mutahaba,” anasema. Ruge amkutanisha na Lady Jaydee “Nilipofika, nilikuta kambi imeshaanza siku mbili zilizopita, hivyo aliyekuwa anasimamia aliniambia sitaweza kupata nafasi ya kushindana. “Nikaomba nipande jukwaani tu kuburudisha. Baada ya kushuka jukwaani, marehemu Ruge aliniita na kuniambia alikuja Zanzibar kwa ajili yangu kwa kuwa alisikia taarifa zangu kutoka kwa mwanzilishi wa Chuchu Sound, Yusuf Chuchu. “Kwa mara ya kwanza marehemu Ruge alinipatia Sh laki moja kwa ajili ya nauli na kuniambia kesho yake niende Dar es Salaam nitamkuta katika Jengo la Kitega Uchumi,” anasema Hammer Q. Akiwa chini ya lebo ya Simoti Vibe ya Ruge, ndipo alipoanza kufanya kazi na Ray C, Lady Jeydee, Man Dojo na wengine. “Ngoma yangu ya kwanza ilikuwa ‘Jamila’ lakini haikutamba sana ila niliifanyia shoo wakati msanii Sean Paul alipokuja kwa mara ya kwanza nchini,” anasema na kuongeza: “… Baada ya hapo, nilishauriwa na marehemu Ruge niimbe taarabu kutokana na mvuto wa sauti yangu. Ndipo nikaimba ‘Pembe la Ng’ombe’ ambayo ilitamba sana.” Hata hivyo, baada ya Simot Vibe kubadilishwa jina na kuwa THT, aliletwa mwalimu raia wa Zaire, Mangu Stino, ambaye hata hivyo waliishia kugombana, hivyo Hammer Q ‘kusepa’ zake. Afunguka kilichoivunja ndoa yake Ukimuuliza Hammer Q juu ya changamoto alizokumbana nazo katika muziki, atakutajia ndoa yake ya mwaka 2013 na mwanamuziki mwenzake wa Taarab, Salha, ambapo walibahatika kupata mtoto wa kiume. “Mke wangu ilikuwa tukigombana kidogo anakwenda kwa waandishi wa habari na kuanza kunianika kwenye redio na magazeti kwa sababu ya umaarufu wangu. Hivyo nikaona niachane naye tu,” anasema. Asema anaudai muziki Akizungumzia kupotea kwake kwenye muziki, anasema muziki umebadilika tofauti na enzi alizokuwa akitamba. Pia, alikatishwa tamaa na baadhi ya vyombo vya habari kwa kutocheza ngoma zake kwa sababu wanazozijua wenyewe. “Nafanya zaidi muziki wa bendi, naimba katika hoteli mbalimbali za kitalii,” anasema Hammer Q na kuongeza kuwa pia amekuwa akitupia kazi zake katika mtandao wa Youtube. Juu ya faida aliyopata kutokana na muziki, anasema hakuna alichoambulia, hivyo hadi sasa anaudai muziki, akiamini ipo siku utamlipa kwa kuwa ni kazi anayoitegemea kuendesha maisha yake. Aliiambia safu hii kwa sasa anaishi Kimara, Dar es Salaam, ambapo mbali ya kuimba pia ni prodyuza katika studio yake iliyoko huko. Anaongeza kuwa ana ngoma nyingi nzuri lakini hawezi kuzitoa kwa sababu hana mtu wa kumsimamia. “Muziki unahitaji mtu wa kukusimamia, si tu kifedha, bali awe na njia mbadala nyingi. Siwezi kutoa nyimbo zangu zikapotelea njiani,” anasema Hammer Q, akisisitiza kuwa anahitaji mtu wa aina hiyo.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 132783


<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>