NA
MICHAEL MAURUS
WAPINZANI
wa Yanga katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Zesco
United ya Zambia, leo itashuka dimbani kucheza na Zanaco, ukiwa ni mchezo wa
Ligi Kuu ya kwao, huku Wanajangwani wakizidi kurahisishiwa kazi kuelekea kipute
chao.
Mchezo
huo wa Zesco na Zanaco ambao ni wa ufunguzi wa ligi, utapigwa kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola,
huku wapinzani hao wa Yanga wakiwa ndio wenyeji.
Hivyo,
leo itakuwa ni nafasi adimu kwa Yanga kuwasoma Zesco kutokana na ukweli kwamba
wapinzani wao hao watalazimika kutumia mbinu zao zote kupata ushindi ili kulipa
kisasi cha kufungwa mabao 4-1 na Zanaco msimu uliopita.
Ukiachana
na hilo, Yanga wamepata zali lingine kuelekea mchezo wao na Zesco baada ya
washambuliaji wawili wa mabingwa hao wa Zambia kuchonganishwa hali
itakayowafanya kutokuwa na ushirikiano unaostahili kila mmoja akisaka ufalme,
hiyo ikiwa ni faida kwa kikosi cha Mwinyi Zahera.
Beki
wa Sofapaka ya Kenya, George Maelo ndiye ‘aliyemwaga upupu’ katika safu
ya ushambuliaji ya Zesco akiwachonganisha Jesse Were na straika mpya wa timu
hiyo raia wa Uganda, Umaru Kasumba.
Maelo
amemwabia Were kuwa Kasumba ametua Zesco inayonolewa na kocha wa zamani wa
Yanga, George Lwandamina, kumaliza ufalme wake kwani Mganda huyo ni hatari kwa
kucheka na nyavu.
“Kasumba
ni mshambuliaji hatari, naamini atamfunika Were na kumaliza ufalme wake Zesco,
cha msingi ampe ushirikiano,” alisema Maelo raia wa Kenya.
Were
alijijengea ufalme ndani ya Zesco United akiwa kama mpachikaji wao mahiri wa
mabao na kwamba Maelo anadhani mchuano wa kuwania umwamba wa kufunga baina ya
washambuliaji hao, utakuwa mkali.
Kutokana
na hilo, ni wazi Were hatakuwa tayari kumpa ushirikiano Kasumba kuepuka kuporwa
ufalme wake mbele ya mashabiki wa Zesco, hiyo ikiwa ni faida kubwa kwa timu
pinzani, wakiwamo Yanga kuelekea mechi baina yao na wababe hao wa Zambia,
Septemba 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wakati
huo huo, Yanga imetuma mashushushu mjini Ndola kwenda kushuhudia mechi kati ya
Zesco na Zanaco, ikiwa ni sehemu ya kuzisoma mbinu za Lwandamina.
Kiongozi
mmoja wa Yanga, ameliambia BINGWA kuwa watu wao walioondoka nchini jana
asubuhi, wataipeleleza Zesco katika kila idara na watakaporejea, kumkabidhi
ripoti kocha wao, Zahera.
“Hilo
ni kweli ila siwezi kukutajia majina ya watu tuliowatuma Zambia, siku hizi
mitandao imeharibu kila kitu, chochote kinachotoka kwenye vyombo vya habari,
sekunde tu, kimeenea dunia nzima,” alisema kiongozi huyo ambaye hakupenda
kutajwa jina.
Kikosi
cha Yanga baada ya kuitoa Township Rollers ya Botswana katika hatua ya awali,
kinatarajiwa kujichimbia jijini Mwanza kukisuka zaidi kikosi chao tayari kumtoa
nishai Lwandamina.
↧