Quantcast
Channel: Magazeti ya Tanzania - Tanzania Newspapers | Magazetini
Viewing all articles
Browse latest Browse all 132783

Ingekuwaje Tulia angekuwa spika?

$
0
0
TANGU Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, arejee kutoka India alipokuwa akitibiwa; matumaini yameibuka ya kupatikana suluhu ya mgogoro wa kisiasa unaoendelea bungeni, mgogoro uliosababisha wabunge wa vyama vya upinzani kususia mkutano wa bunge lililopita,  la bajeti. Akijiandaa kurudi kazini, katika mkutano ujao unaotarajiwa kuanza Septemba 5, Ndugai amekaribisha mazungumzo ya kutafuta muafaka na wapinzani. Amewasihi wabunge wa upinzani kurudi bungeni na kueleza mambo yaliyowaudhi ili wakae wajadili na watafute ufumbuzi badala ya kuendelea kususia. Ndugai alikiri kuwa hali ya sasa ya bunge hairidhishi kutokana na machafuko ya kutoafikiana baina ya kambi ya upinzani (KUB) na wabunge wa chama tawala kiasi cha kusababisha wabunge wa upinzani kususia bunge lote lililopita. Alisema: "Wabunge kutoka nje ni jambo ambalo halipendezi hata kidogo, nisingependa niendelee kuliona. Nawaomba katika bunge lijalo kama wanahisi tunakosea watueleze, na sisi tuwaeleze wanakosea wapi ili twende sawa. Kisha Ndugai akanukuliwa tena gazeti moja la kila siku akisema amefikiria kuunda kamati ya maridhiano itakayojumuisha maspika wa zamani, kwa ajili ya kujadiliana na pande zote mbili za wabunge kwa maana ya wapinzani na chama tawala, ili kutengeneza bunge lenye maridhiano. Juhudi za Ndugai za  kuleta maelewano zinaibua matumaini kuwa kumbe licha ya CCM kutawaliwa na siasa za ubabe na kuwakomoa wapinzani; kuna wachache, ndani ya chama hicho, wenye fikra zilizotulia na wanaofikiri sawa sawa na bila jazba, kama Spika Ndugai. Kwamba sauti ya busara na matumaini yameibuka kutoka kwa spika ya  bunge, akiongoza kati ya mihimili mikuu mitatu ya utawala, inaleta faraja kubwa katika kipindi hiki cha giza la demokrasia. Kauli za Ndugai zinatia faraja zaidi kwa sababu, kwa sasa, kila kiongozi wa serikali na CCM anajitahidi kuzungumza kibabe dhidi ya wapinzani, akimuiga Magufuli, katika harakati za kujipendekeza. Ndugai, yeye, ameenda kinyume na msimamo wa kundi la wana CCM wengi – kundi la bendera fuata upepo – linalounga mkono siasa za wakati huu, siasa za ‘ki – Magufuli’. Katika kundi hilo yumo pia msaidizi wa Ndugai  Dk. Tulia Ackson.  Dk. Tulia hawezi kuepuka lawama katika yaliyojitokeza bungeni na kusababisha wapinzani kususia. Ukiacha shutuma za moja kwa moja dhidi yake, zilizowasilishwa kwa spika kimaandishi, akilaumiwa kwa kupendelea upande mmoja; Tulia aliendelea kufanya makosa yaliyotanua mgogoro huo. Kosa kubwa la Tulia ni kuangalia tatizo la kisiasa kwa jicho la sheria pekee. Siasa zinaendeshwa na sheria, lakini siasa ni siasa. Kuna wakati inakubidi uchepuke kutoka katika sheria na kutafuta majawabu ya kisiasa ya tatizo la kisiasa linalokukabili. Tulia, alizingatia usahihi wa masimamo wake kisheria pekee na kupuuza malalamiko ya wapinzani. Dk. Tulia pia hakuzingatia maslahi ya taifa na badala yake akaendeleza mpango wa kukomoana. Hilo linathibitika pale alipoamua kukalia kiti hicho kwa siku nyingi mfululizo yeye mwenyewe bila kumkaimsha mtu yeyote ili tu aendelee kuwaudhi na kuwakomoa wapinzani. Katika kipindi hicho chote, wapinzani waliendelea kutoka nje na hivyo mjadala ukaendelea wa upande mmoja, katika kipindi muhimu cha bajeti. Dk. Tulia alikuwa akifurahia kuwakomoa wapinzani akisahau kuwa taifa linaumia kwa watu wengi kukosa uwakilishi katika mijadala muhimu ya bajeti. Mijadala ya upande mmoja iliyoendelea bungeni ilisererekea katika kashfa na vijembe dhidi ya waliotoka, jambo ambalo Dk. Tulia alionekana kulilea. Ulikuwa ni ushindi mkubwa wa kisiasa kwa Dk. Tulia na CCM, lakini taifa lilipata hasara.  Msimamo wa Dk. Tulia wa kupuuza wapinzani ndio msimamo wa serikali ya awamu ya tano. ‘Hakuna maandamano,’ ‘mikutano ya hadhara marufuku,’ ‘bunge lisioneshwe moja kwa moja’ – na hakuna mjadala kuhusu uamuzi huo. Sisi ndio wenye mamlaka. Chukua au acha.”  Wakati amefanikiwa kufanya apendeke mbele ya mkuu wa nchi, ambaye ndiye aliyemteua kuwa mbunge ili apate sifa ya kugombea unaibu spika, kwa upande mwingine Dk. Tulia amewaangusha watu wengi waliokuwa na matumaini naye- ikiwemo vijana, wanawake na wasomi. Anayoyafanya sasa Job Ndugai ndiyo aliyopaswa kuyafanya Dk. Tulia muda mrefu – yaani kuwanyoshea mkono wapinzani na kuwakaribisha kwa ajili ya maongezi, ikiwezekana kushirikisha wenye busara ndani ya bunge, ili kupata suluhu ya mgogoro.  Dk. Tulia alipopuuza kususa kwa wapinzani na kung’ang’ania kuendesha bunge katika wingu la shaka ya upande mmoja kukosa imani naye, ni sawa na kusema yeye ni muhimu kuliko taifa. Ni bora mijadala muhimu ya kitaifa ikwame lakini yeye abaki na unaibu spika.  Vipi ingekuwa Tulia ndiye spika kamili? ENDS  

Viewing all articles
Browse latest Browse all 132783

Trending Articles