DORTMUND, Ujerumani
HISTORIA inaonesha kwamba timu iliyoweza kufanya makubwa ikiwa na vijana wadogo ilikuwa ni Manchester United ya msimu wa 1995/96, ambayo hata hivyo ilianza Ligi kwa kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Aston Villa.
Matokeo hayo yalimuibua mchambuzi wa soka wa kipindi hicho, Alan Hansen, aliyedai kwamba United isingeshinda taji lolote iwapo wangeendelea kuwaamini vijana wadogo.
Lakini vijana hao; Paul Scholes, David Beckham, Nicky Butt, ndugu wawili, Gary na Phill Neville, ambao Hansen aliwaona si lolote, ndio walioipa United taji la Ligi Kuu na FA.
Klabu ya Borussia Dortmund inaelekea kidogo kufanana na Man United ya 1995/96. Iliuanza msimu bila kuaminika na wengi kutokana na rekodi yao ya kumaliza msimu uliopita katika nafasi ya nne.
Pia wengi wao waliamini baada ya Dortmund kuwauza nyota wao muhimu kama vile Pierre-Emerick Aubameyang, Sokratis Papastathopoulos na Ousmane Dembélé ndani ya miezi 12 tu, timu hiyo isingeweza kufurukuta tena mbele ya Bayern Munich.
Hata hivyo, ni mechi 11 zimeshachezwa hadi sasa kwenye Bundesliga, Dortmund ya vijana haijapoteza mchezo wowote na wikiendi iliyopita waliibuka wababe kwa kuitandika Bayern Munich mabao 3-2.
Dortmund iliyobezwa awali, hivi sasa ndiyo inayoshikilia usukani wa Bundesliga, ina safu ya mashambulizi inayotisha kwa mabao na mabeki wasiopitika kirahisi.
Katika jumla ya wachezaji 17 walioitumikia Dortmund kwa zaidi ya dakika 200 za mechi kwenye Bundesliga msimu huu, ni wachezaji tisa wenye umri wa miaka 23 au chini ya hapo.
Watano kati ya hao 17, wana miaka 20 au chini ya hapo, na ni nyota watatu tu ambao wameshafikisha umri wa miaka 29 kwenda juu.
Kifaa muhimu katika kesi hii ya Dortmund kuwa ya moto msimu huu kama Man Utd ya miaka zaidi ya 20 iliyopita, ni uwepo wa mshambuliaji mzoefu na tegemeo.
Pia, mchezaji huyo ni yule mwenye uwezo mkubwa wa kuwaongoza vijana wadogo na kuwaonesha mfano wa kupambana katika mechi muhimu za kusaka mafanikio.
Katika timu ya United msimu wa 1995/96, alikuwapo Eric Cantona; lakini kwa Dortmund ya msimu huu, yupo mtu mmoja aitwaye Marco Reus.
Gary Neville aliwahi kusema kwamba, kipindi hicho walimtegemea mno Cantona kwa sababu alikuwa mkubwa wao, mzoefu na mchezaji asiyetaka kushindwa.
Lakini kama Dortmund itahitaji kufanya makubwa msimu huu ikiwa na vijana, ni lazima wachezaji hao ambao kiumri bado ni wachanga, watatakiwa kumtazama Reus.
Ikumbukwe kuwa, Cantona alichelewa sana kuuanza msimu wa 1995/96, kwani ilimbidi asubiri hadi adhabu aliyopewa kutokana na kitendo cha kumtandika shabiki wa Crystal Palace teke iishe, ndipo alipoweza kuanza kucheza kuanzia mwezi Oktoba.
Pindi United ilipocheza mechi za Ligi kwa miezi miwili bila uwepo wa Cantona, klabu ya Newcastle United ndiyo iliyokuwa ikiongoza msimamo.
Baada ya kurejea kwa Cantona, hadi kufikia Januari 1996, United ilifanikiwa kupunguza pengo lote la pointi 12 na kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.
Hata hivyo, Reus yeye hajaanza kama Cantona, ameshacheza mechi 16 za michuano yote kwa upande wa timu yake ya Dortmund, akifunga mabao 10 na kutoa pasi nne za mabao.
Lakini hatutakosea kusema kwamba ni kama tunamwona Reus akifanya makubwa tuliyoyatarajia muda mrefu uliopita, hatukuwa na ndoto ya kumwona nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 akiwa wa moto msimu huu.
Kwa muda mrefu, Reus amekuwa akisumbuliwa na majeraha mabaya ambayo yalituaminisha kuwa mshambuliaji huyo angepotea kwenye ramani ya soka, lakini mpaka kufikia hivi sasa, ameweza kucheza dakika nyingi kuliko misimu miwili iliyopita.
Hilo tu linatosha kumwelezea Reus ambaye ni nahodha wa Dortmund kwamba ndiye mchezaji anayefaa kuwaongoza makinda wanaoipaisha timu hiyo msimu huu.
Ukimtazama Reus anavyocheza msimu huu, utagundua kwamba nyota huyo amekuwa binadamu mwenye presha ya kudhihirisha bado uwezo wake ni mkubwa, akizingatia umakini, huku akijua wazi lolote atakalofanya uwanjani litakaribisha hali ya kuwa majeruhi.
Heshima anayopata Reus kutoka kwa vijana wa timu ya Dortmund, ni sawa na ile ambayo Cantona alikutana nayo Old Trafford.
“Reus ni mfano wa kuigwa kwangu kwa sababu ni mchezaji mkubwa,” alisema winga, Jadon Sancho, alipohojiwa na kituo cha Deutsche Welle.
Kiufundi, Reus amekuwa na msaada mkubwa Dortmund kutokana na uamuzi wa kocha wake, Lucien Favre, kumbadilisha kutoka kuwa mshambuliaji wa pembeni kushoto, na kumtumia kama namba 10.
Hapo Reus ana jukumu la kuwachezesha washambuliaji vijana na wenye njaa ya mafanikio katika timu hiyo, wanaofunga mabao na kushirikiana kama siafu.
Reus amekuwa na uhuru wa kuzunguka katikati mwa safu ya ulinzi na viungo wa timu pinzani, pia kuzalisha nafasi za kufunga mabao baada ya wenzake kufanya kazi kubwa kama vile kupokonya mpira.
Ni sawa na alivyokuwa Cantona wa United ya msimu wa 1995/96.
Dortmund ilipoitandika Bayern katika dimba la Signal Iduna, Sancho alikuwa akiwadhalilisha mno mabeki wa miamba hao.
Jacob Bruun Larsen, mwenye umri wa miaka 20, alikuwa ni mbunifu na mchapa kazi, huku Achraf Hakimi, 19, yeye alikuwa mtulivu zaidi.
Lakini, aliyetikisa zaidi ni Reus, ambaye licha ya kufunga mabao mawili, kazi kubwa aliyoifanya ni kulainisha vyuma vyote vilivyokaza siku hiyo.
The post MFALME Reus wa Dortmund anatukumbusha Cantona wa Manchester United appeared first on Bingwa.
↧