KIGALI, RWANDA
SHIRIKA la usafiri
wa ndege la nchini Rwanda, limetoa agizo kwa marubani na kampuni za ndege
kutoendesha ndege za Boeing 737 Max 8 ama 9 katika anga ya nchi hiyo.
Uamuzi huo wa
Rwanda unamaanisha nchi hiyo imejiunga na mataifa mengine duniani ambayo yamepiga
marufuku usafiri wa ndege hizo aina ya Boeing 787 Max 8 na Max 9.
Hii inafuatia
ajali ya ndege ya Ethiopia Airlines wiki iliyopita ambapo ilianguka muda mfupi
baada ya kupaa kutoka mji mkuu Addis Ababa na kusababisha vifo vya watu 157.
Taarifa zinaeleza
kwamba, Rwanda ilikuwa na mipango ya kukodisha ndege mbili za aina hiyo Boeing
737- 800. Hata hivyo, huenda mipango hiyo ikasitishwa kwa muda sasa wakati
kukisubiriwa uchunguzi wa chanzo cha ajali ya ndege ya Ethiopia iliyoanguka nje
kidogo ya mji mkuu Addis Ababa.
Ndege kama hiyo ya
kampuni ya Lion Air, ilianguka kutoka pwani ya Indonesia Oktoba mwaka jana na
kusababisha vifo vya watu 189. Katika taarifa rasmi iliyowekwa kwenye mtandao
wa twitter ya mkurugenzi mkuu katika shirika hilo la usafiri wa ndege Rwanda,
Silas Udahemuka, RCAA limesema kwamba marufuku hiyo imeanza kufanya kazi mara
moja.
“Shirika la
usafiri wa ndege Rwanda kwa uwezo uliopewa katika kifungu cha 16 cha sheria za
usafiri wa ndege nchini inaagiza marubani na kampuni za ndege zinazohudumu
ndege za Boeing 737 – 8 Max na Boeing 737 – 9 Max, zisiendeshe usafiri wowote
wa ndege hizo katika anga ya Rwanda mara moja,” inasema taarifa hiyo.
Marekani hivi
karibuni imesitisha usafiri wa ndege hiyo ya Boeing 737 Max yakiwemo mataifa
mengine kama Uingereza, Umoja wa Ulaya, China, India na Australia ambayo yote
yameamua kusitisha usafiri wa ndege hizo.
Ndege zote za
Boeing 737 Max 8 na 9, zimepigwa marufuku kuhudumu hadi angalau Mei baada ya
ajali hiyo ya shirika la ndege la Ethiopia, Shirika la kitaifa la usafiri wa
ndege nchini Marekani (FAA).
“Ndege hizo hazitahudumu
hadi mfumo wake wa uhudumu uimarishwe na uidhinishwe,” imesema FAA.
Mkasa huo wa ndege
nje kidogo ya mji mkuu Addis ulisababisha vifo vya watu 157 kutoka mataifa 35. Ni
ajali ya pili ya aina hiyo ya ndege ya 737 Max katika muda wa miezi mitano.
Baadhi ya watu
wamegusia ufanano wa mikasa hiyo, huku baadhi ya wataalamu wakitaja data ya
satelaiti na ushahidi kutoka eneo la mkasa kuonyesha uhusiano wa ajali ya ndege
ya Ethiopia na ile iliyotokea Indonesia ya Lion Air mwaka jana.
Wachunguzi nchini
Ufaransa wamepokea jukumu la kisanduku kinachonakili data ya safari hiyo ya
ndege maarufu ‘black boxes’ wakijaribu kubaini chanzo cha ajali ya ndege hiyo
ya Boeing 737 Max. Huenda ikachukua muda kupata data ya awali, lakini mengi
itategemea hali ya kisanduku hicho.
↧