NA HUSSEIN OMAR
KOCHA wa zamani wa Yanga na timu ya soka ya
Tanzania, Taifa Stars, Mbrazili Marcio Maximo, ameibuka na kuwataka wanachama
wa klabu hiyo kumpigia kura mgombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Fredrick
Mwakalebela, katika uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho.
Maximo anayejishughulisha na shughuli zake binafsi hivi
sasa nchini Brazil, aliwahi kukinoa kikosi cha Yanga msimu wa mwaka 2014 chini
ya uongozi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji.
Ikumbukwe wakati akikinoa kikosi cha Stars mwaka
2006 hadi 2010, Maximo aliwahi kufanya kazi na Mwakalebela kipindi hicho akiwa Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Akizungumza na BINGWA jana, Maximo amewatakia
wanachama wa Yanga uchaguzi mwema, huku akiwasisitiza kumchagua Mwakalebela
kwani utendaji wake wa kazi unafahamika kwa kila mdau wa soka hapa nchini.
“Nimefurahi kusikia Yanga wanafanya uchaguzi na
Mwakalebela ni miongoni mwa wagombea, naomba wanachama wafanye uamuzi sahihi
kwa kuchagua viongozi sahihi,’’ alisema Maximo.
Aidha, aliwasihi wanachama wa Yanga wachague watu wa
mpira kwani klabu hiyo ina rasilimali nyingi za kuifanya iweze kuwa tajiri kama
ilivyo TP Mazembe ya DR Congo na klabu nyingine barani Afrika.
Maximo alikwenda mbali zaidi na kusema wakati
alipokuwa akiinoa Yanga alitamani kuona klabu hiyo inamiliki uwanja wake na
kituo cha soka, lakini ilishindikana kutokana aina ya viongozi waliokuwepo.
“Nilipigania kuanzishwa kituo cha michezo ambacho
kingesaidia kupatikana  wachezaji wengi
vijana watakaocheza timu kubwa na pengine baadaye wangeuzwa, lakini
nilishindwa,’’ alieleza Maximo.
Wakati huo huo, mgombea huyo jana aliendelea kufanya
kampeni na kuwataka wanachama watakaopiga kura kesho kumchagua kwani anajua
kitu ambacho Wanayanga wanakitaka.
“Mimi sina mengi ila nipewe nafasi nifanye kwa
vitendo, naomba wanachama wote wa Yanga waliopo mikoani na kwingineko wajitokeze
kwa wingi kesho wapige kura za ndiyo kwangu,’’ alisema Mwakalebela.
↧