NA WINFRIDA MTOI
LICHA ya kuanza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ushindi
wa mabao 3-1 dhidi ya JKT Tanzania, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, bado
anaumiza kichwa juu ya kikosi chake.
Simba iliibuka na ushindi huo katika mechi
iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Aussems alibadilisha
kikosi chake tofauti na kile kilichoonekana michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa
Afrika na Ngao ya Jamii walipokutana na Azam FC na kuibuka kidedea, wakishinda
mabao 4-2.
Moja ya sababu iliyomfanya Aussems kubadili
kikosi ni kutokana na baadhi ya nyota wake kama Shomari Kapombe, John Bocco na
Pascal Wawa kuwa majeruhi, huku Jonas Mkude akisumbuliwa na homa.
Wekundu wa Msimbazi hao walianza ligi wakiwa
tayari wameondolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na UD Songo ya Msumbiji
iliyosonga mbele kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutokana sare ya 1-1,
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mechi ya awali wakitoka suluhu nchini kwao.
Kitendo hicho kiliwafanya Simba kupania ligi
kuu kwa sababu ndiyo michuano pekee itakayowarudishia heshima yao endapo
watafanya vizuri na kutetea ubingwa wao.
Kutokana na hilo, matarajio ya benchi la
ufundi ilikuwa ni kuanza kwa ushindi wa mabao mengi zaidi ya matatu
waliyoifunga JKT Tanzania.
Kauli ya Aussems baada ya mechi hiyo
ilidhihirisha kuwa lengo lake halijatimia kwa kusema walistahili kushinda mabao
mengi zaidi ya 3-1.
Kocha huyo aliweka bayana kutoridhishwa na
matokeo na uchezaji wa nyota wake kwa kile alichodai dakika za mwisho,
walionekana wakicheza kama watoto.
“Katika mchezo huu tulitakiwa kushinda mabao
mengi zaidi, sijaridhika kwa nafasi na kikosi nilichopanga, tulitakiwa kufunga
mabao manne hadi sita, ila kuna makosa na dakika 15 za mwisho tulicheza kama
watoto,” alisema.
Alieleza kuwa kuelekea mechi zijazo,
ataendelea kuwandaa wachezaji wake kisaikolojia ili kusahau matokeo yaliyopita ya
kutolewa katika michuano ya kimataifa, akiamini itasaidia kufanya kile
anachohitaji.
↧