Quantcast
Channel: Magazeti ya Tanzania - Tanzania Newspapers | Magazetini
Viewing all articles
Browse latest Browse all 132783

CUF – aliyewatosa wakati muhimu hafai kurejeshwa uongozini

$
0
0
NA HILAL K SUED, PROFESA Ibrahim Lipumba, mwanasiasa maarufu nchini na msomi aliyebobea katika masuala ya uchumi amekiongoza Chama cha Wananchi (CUF) kwa takriban miaka 20 – tangu 1995. Aidha, amegombea urais kupitia chama hicho mara nne – kuanzia uchaguzi wa mwanzo chini ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1995. Na katika mara zote hizo ni uchaguzi wa mwaka 2000 na 2005 ndiyo alifanya vizuri kwa kuwa wa pili nyuma ya CCM baina ya wagombea kadha waliokuwemo katika kinyang’anyiro katika nafasi hiyo. Kwa ujumla katika kipindi cha uongozi wake, CUF ilifika kileleni kiufuasi na kiumaarufu kati ya 2000 na 2005, na baada ya hapo kikaanza kupokonywa umaarufu na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ingawa kule Visiwani CUF iliendelea kuwa chama tishio kwa chama tawala – CCM. Profesa Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa chama hicho Agosti mwaka jana kutokana na kile alichokiita kusutwa nafsi yake baada ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), muungano wa vyama vya upinzani ulioanzishwa wakati wa mchakato wa kupata katiba mpya – kumteua Edward Lowassa kuwa mgombea pekee kutoka muungano huo. Ikumbukwe kwamba ilikuwa ni kutokana na ushawishi mkubwa wa Profesa Lipumba kuunda UKAWA kwa lengo la kuweka msimamo mmoja wa upinzani katika kupata Katiba mpya inayodaiwa na wananchi na ni yeye ndiye aliyebuni jina hilo. Hata baada ya mchakato wa kuandika Katiba mpya ulipomalizika mwishoni mwa 2014 na UKAWA kuzidiwa na upande wa CCM, viongozi wa upinzani waliendelea na mshikamano wao chini ya mwamvuli wa UKAWA na kuahidi kwamba umoja huo ni wa kudumu na hata kuahidi kwamba upinzani unafikiria kushiriki uchaguzi wa mwaka 2025 chini ya umoja huo. Ilikuwa ni habari njema kwa upande wa upinzani kwani wengi waliona kwamba sababu mojawapo kubwa kwa CCM kuendelea kukaa madarakani ni kukosekana umoja katika kambi hiyo. Na hakika, CCM ilikuwa inafanya kila mbinu, hila na ghilba kuhakikisha upinzani unabakia kama ulivyokuwa — katika mgawanyiko. Kwa ujumla wafuasi katika kambi ya upinzani waliukumbatia umoja wao huo – na hasa baada ya mkutano mkuu wa hadhara wa vyama vya umoja huo – CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD – uliofanyika katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam miezi michache kabla ya uchaguzi ambao uliweka maazimio kadha ya, pamoja na ahadi ya kugombea uchaguzi kipamoja – na hayo yalitiwa sahihi uwanjani hapo na makatibu wakuu wa vyama hivyo. Nimeona umuhimu wa kuweka utangulizi huu kutokana na kile kilichotokea kuelekea uchaguzi mkuu kwamba baadhi ya viongozi wa umoja huo hawakuwa wameukumbatia umoja huo kwa dhati – au labda niseme kwamba walikuwa rahisi kuyumba au kuyumbishwa kwa jambo lisilo na msingi kabisa. Kwa jinsi hali ilivyokuwa ikionekana na Profesa Lipumba kupaswa kufahamu ni kwamba katika umoja huo yeye alikuwa anacheza zumari Namba 2 (second fiddle) kutokana na ufuasi wa vyama vya upinzani, na hali hii ilikuja chini ya uongozi wake katika CUF – yaani kukiruhusu chama chake kupitwa na Chadema. Bila shaka kuna mengi alipaswa kufikiria hapo – kwa nini ilikuwa hivyo. Hivyo hatua ya kujiondoa uongozi wa chama hicho katika dakika za mwisho, ambapo uwepo wake ulikuwa muhimu na kuhitajika sana kupita wakati wowote wa harakati za upinzani hapa nchini na hivyo ni vigumu kuamini haikuwa usaliti. Sababu kuu aliyotaja wakati anajiuzulu ni kwamba kada maarufu wa CCM na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu aliyehamia Chadema na kupendekezwa kuwa mgombea urais wa UKAWA hafai kwa sababu alikuwa anapinga upatikananaji wa Katiba chini ya Rasimu ya Jaji Warioba wakati ule wa mchakato. Nasema hivi kwa sababu ya ile ‘timing’ – kwani kwa namna chama tawala kilivyokuwa kinabanwa jinsi uchaguzi ulivyokuwa unakaribia, ilitakiwa ‘msukumno’ mmoja tu wa mwisho (one final heave) wa kipamoja kukiondoa chama hicho madarakani kupitia   sanduku la kura. Hayati Nkwame Nkrumah, katika harakati zake za kudai uhuru wa Ghana miaka ya 1950 alijitahidi sana kuwaweka viongozi wenzake katika mstari mmoja baada ya kuona wakiyumbishwa. Aliwaambia: “Pateni ufalme wa dola kwanza.” (“Seek ye political kingdom first”). Alimaananisha baada ya kushika dola mengine yote yangelifuata. Hivyo madai makuu ya Profesa Lipumba kuhusu Katiba mpya yangepatikana mara moja iwapo tu angebakia katika Ukawa na kuusaidia umoja huo kushika dola. Sote tunafahamu kwamba Katiba mpya inayotakiwa na wananchi haiwezi kupatikana chini ya CCM. Aidha, hakuna haja ya kusema kwamba kitendo cha kujitoa dakika hizo mwisho kilikifurahisha chama tawala na sitakosea uiwapo nitsema viongozi wa chama hicho walikuwa wanaambizana: “Si unaona, wameanza kusambaratika.” Ni kitendo kilichowatia wafuasi wengi huzuni na kuwaweka njia panda, na wengine hata kuhamia au kurejea CCM baada ya kuona mvurugano huo, hasa kikijumlishwa na kile kitendo cha Dk. Willibrod Slaa, Katibu Mkuu wa Chadema naye kujiondoa kutoka UKAWA – ingawa yeye zaidi alitaja masuala ya msingi zaidi – ya ufisadi – kwamba aliwahi kumtuhumu Lowassa kwa ufisadi, tena hadharani. Iliumiza zaidi hasa pale Profesa Lipumba alionekana kushiriki vikao vilivyokuwa vikimjadili ujio wa Lowassa katika Ukawa. Kwa mtazamo wangu Dk. Slaa alikuwa angalau ana hoja ambayo iliwezekana kweli ilimsuta, ingawa naye kitendo chake cha kujiondoa dakika za mwisho kiliwapa sana faraja ‘adui’ yake mkubwa wa siku zote – CCM. Ni vigumu kufahamu kuondoka kwa Profesa Lipumba kutoka UKAWA kuliuumiza umoja huo kwa kiwango gani katika uchaguzi mkuu wa 2015 – bara na visiwani. Sasa hivi kuna tetesi kwamba Lipumba anaihitaji tena nafasi yake ya uenyekiti wa CUF, ingawa binafsi sijamsikia yeye akitamka hivyo kwa bayana. Inawezekana ameanza kutanguliza wapambe wake kupima joto. CUF itakuwa inafanya makosa makubwa iwapo itamrejesha kwenye uongozi mtu ambaye wakati alipokuwa akihitajika sana chamani yeye aliamua kukitosa. The post CUF – aliyewatosa wakati muhimu hafai kurejeshwa uongozini appeared first on Gazeti la Rai.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 132783


<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>