MWANDISHI WETU
MWANZONI mwa wiki hii Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam, ilitengua uteuzi wa wajumbe wa bodi ya chama cha Wananchi –CUF
iliyoteuliwa na Mwenyekiti wake, Ibrahim Lipumba.
Wajumbe hao wa bodi walipendekezwa na Prof. Lipumba
ambaye hana uhusiano mzuri wa kikazi na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif
Hamad tangu Agosti 6, 2015 mara baada ya msomi huyo wa uchumi kutangaza
kujiuzulu nafasi yake ya uenyekiti.
Hata hivyo Prof. Lipumba alijirejesha kwenye nafasi
yake hiyo mwaka mmoja baadae na kuteua bodi ya wadhamini waliosajiliwa na
Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita) kama ilivyoelekezwa katika sheria
namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992.
Uamuzi huo umetazamwa kama ushindi kwa kambi ya
Maalim Seif na huku ukibeba dhana ya kushindwa kwa kambi ya Prof. Lipumba.
Kwa miaka minne sasa CUF imekuwa ndani ya mgogoro
mzito wa kiuongozi, hali inayochagiza kuwapo kwa kesi za mara kwa mara kati ya
pande hizo mbili.
Mara baada ya kutolewa kwa hukumu ya kesi hiyo ya
kuwapinga wajumbe wa bodi ya chama hicho, iliyofunguliwa na Mbunge wa Malindi,
Ally Salehe, kesho itatolewa hukumu nyingine dhidi ya uhalali wa Prof. Lipumba
kuwa mwenyekiti baada ya kutangaza kujiuzulu.
Prof. Lipumba alitangaza uamuzi huo kwa kile
alichodai kuwa ni kutoridhishwa na uamuzi wa vyama vilivyounda Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa) kumpitisha Edward Lowassa kuwania tiketi ya urais.
Endapo hukumu inayotarajiwa kutolewa kesho na
Mahakama hiyo hiyo iliyotoa uamuzi wa kutengua uteuzi wa wajumbe wa bodi,
itaharamisha uhalali wa Prof. Lipumba kwenye nafasi ya uenyekiti ni wazi wiki
hii itakuwa mbaya kwa mwanasiasa huyo.
Uamuzi wowote ambao hautakuwa na maslahi kwa
Lipumba, utaibua mjadala mzito na kuhalalisha malalamiko ya muda mrefu ya
baadhi ya makada wa CUF upande wa Maalim Seif, wanaodai kuwa mwenzao huyo wa
zamani anabebbwa na serikali.
Tayari kambi ya Maalim Seif imeshaonesha furaha yake
na kuwataka wafuasi wao kuendelea kuwa watulivu ili kile wanachodai kuwa ni
haki yao kipatikane.
“Nawaomba wanachama wa CUF wawe watulivu, wakati
tukisubiri uamuzi mwingine utakaotolewa Ijumaa.”
Ukweli ni kwamba endapo mahakama itatoa uamuzi wa
kuharamisha uenyekiti wa Prof. Lipumba huenda ukawa mwanzo wa uimara zaidi wa
mwanasiasa huyo au akajikuta nje ya ulingo wa siasa za upinzani.
Upo uwezekano mkubwa wa Prof Lipumba kupepesuka na
pengine kujiondoa kabisa kwenye uga huo kama alivyofanya kwa hiyari yake mwaka
2015.
Tayari Maalim Seif ameshamtaka Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi wa fedha za ruzuku za chama
hicho zilizokuwa zikimilikiwa na kambi ya Prof. Lipumba.
Maalim Seif ametaka kufanyika kwa ukaguzi huo kwa
hoja kuwa bodi ya aliyekuwa mshirika wake kisiasa haikuwa halali.
“Tumeupokea kwa furaha uamuzi wa Mahakama Kuu
umekata mzizi wa fitina wa madai yetu dhidi ya Rita, nilishasema tangu awali
tuko tayari kupokea uamuzi wowote wa Mahakama,” alisema Maalim Seif.
CUF
KUREJEA ZANZIBAR
Kabla
na hata baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 CUF ilizatamwa kuwa na nguvu kubwa ya
kisiasa Zanzbibar, hadi pale chama hicho kilipoingia kwenye mgogoro wa wenyewe
kwa wenyewe mwaka 2016.
UUamuzi
wa wiki hii unaweza kurejesha uimara wa chama hicho Zanzibar, hatua
inayoonekana kuwa na matokeo mabaya kwa Prof. Lipumba na washirika wake.
Nguvu
ya chama hicho Zanzibar inatambulika wazi kwani kilishawahi kuingia kwenye
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyoundwa kutokana na mwafaka wa pili kati
ya chama hicho na Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya mgogoro wa kisiasa
ulioibuka kutokana na uchaguzi wa mwaka 2010.
Ujio
wa SUK huku Maalim Seif akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ulichagiza
kuingia serikalini kwa baadhi ya makada wake.
Kwa
vipindi kadhaa huko nyuma CUF ndiyo kilikuwa kama chama tawala kisiwani Pemba
kikiwa na masheha, wawakilishi na wabunge katika Bunge la Muungano.
Kukosekana
katika vyombo hivyo vya maamuzi na uwakilishi Zanzibar pamoja na mgogoro wa
wenyewe kwa wenyewe vinatajwa kupunguza nguvu na ushawishi wa chama.
Uamuzi
wa Mahakama Kuu wa wiki hii unaweza kukiimarisha chama hicho na kudhoofisha
nguvu za kiongozi mmoja mmoja kati ya Maalim Seif na Prof. Lipumba.
The post Ni wiki ya kusimama au kuanguka kwa Lipumba? appeared first on Gazeti la Rai.
↧