MWANDISHI WETU
MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye katika
siku za karibuni alikuwa na ziara katika nchi za Ulaya na Marekani kufanya mahojiano na vyombo
vya habari vya Kimataifa, amerejea tena kitandani wiki hii kufanyiwa upasuaji
wa 23, tangu aanze kupatiwa matibabu Septemba 7, 2017 mara baada ya
kushambuliwa kwa risasi, mkoani Dodoma.
Mara
baada ya kushambuliwa Lissu alikimbizwa Nairobi nchini Kenya na huko ndiko
upasuaji wake wa kwanza ulianzia.
Katika
kipindi cha miezi minne alichokitumia akiwa kitandani hospitalini jijini
Nairobi, Lissu alifanyiwa upasuaji wa maeneo mbalimbali ya mwili wake yaliyoathiriwa
mara 17 na risasi.
Mara
baada ya kupelekwa nchini Ubelgiji katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven,
Campus ya Gasthuisberg, mjini Leuven, Januari mwaka jana Lissu alifanyiwa
upasuaji wa 18 na hadi kufikia Desemba 31, 2018 alishapasuliwa mara 22.
Katika
salamu zake za mwaka mpya wa 2019 Lissu alipata kusema kuwa tofauti na mwanzoni
mwa mwaka jana, mwaka huu anarudi hospitali ili kumalizia safari ndefu ya tiba,
iliyoanzia Hospitali ya Mkoa wa Dodoma siku ya kushambuliwa kwangu.
“Katika operesheni hii ya majuzi (Desemba 31, 2018) , timu ya madaktari bingwa
ambao wamenitibu tangu nilipofika hapa Ubelgiji mapema mwaka jana, imeondoa
kifaa kikubwa cha chuma kilichowekwa ili kuunganisha mfupa wa mguu wangu wa
kulia, ambao uliumizwa vibaya katika shambulio la Septemba 7.”
Akizingumzia
upasuaji wake wa 23, kwenye mahojiano maalumu na kituo cha televisheni cha
Sauti ya Amerika (VOA), Lissu alisema bado hajapona lakini anaendelea vizuri na
upasuaji huu wa wiki hii ndio utamwezesha kujua uimara wa afya yake.
“Siwezi
nikazungumzia nimepona kwa asilimia ngapi, lakini naweza kusema kwamba
naendelea vizuri, sijapona kwa sababu tarehe 20 ya mwezi huu (Februari) naenda
kufanyiwa oparesheni ya 23, kwa hiyo sijapona ila naendelea vizuri,” alisema
Lissu.
Kuhusu
kurudi nyumbani, Lissu alisema siku yoyote daktari wake akimwambia anaweza
kurudi, hatosita na badala yake siku inayofuata atakuwa ndani ya ndege kurejea
Tanzania.
Lissu
ambaye pia ni mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni ametembelea nchi za
Ujerumani, Marekani na Uingereza pamoja na kufanya mahojiano na vituo vya
habari vya Deutsche Welle (DW), Shirika la Habari la Uingereza (BBC) na Sauti
ya Amerika (Voa).
Aidha,
amefanya mihadhara na wasomi wa Chuo Kikuu cha Mambo ya Kimataifa cha Elliot
nchini Marekani.
Kauli
alizopata kuzitoa katika mahojiano aliyoyafanya ziliwaibua wabunge, mabalozi,
viongozi wa Serikali, wakuu wa wilaya na mikoa, viongozi wa Jumuiya za Chama
Cha Mapinduzi na viongozi wa juu wa chama hicho kumjibu na wakati mwingine
kukanusha madai anayoyaelekeza kwa serikali ama viongozi wake.
Wachambuzi
wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa hatua hiyo ya hoja za Lissu kuwaibua watu
mbalimbali wa upande wa Serikali na CCM inatosha kuwa mtaji wa kisiasa kwa
mwanasiasa huyo kusimama kwenye majukwa ya kuwania urais mwakani.
Tayari
Lissu mwenyewe ameshaweka wazi kuwa endapo chama chacke kitampa nafasi hiyo ya
kuwania urais yuko tayari kufanya hivyo kwani anaamini anaweza kufanya vizuri.
Aidha
baadhi ya wafuatiliaji wa siasa nchini wanaamini kuwa huruma ya wananchi wengi
dhidi ya Lissu pamoja na kauli mbalimbali nzito zinazotolewa na CCM na Bunge
zinatosha kumbeba mbunge huyo wa Singida Mahsriki kwenye uchaguzi Mkuu ujao kwa
nafasi yoyote ile atakayoiwania.
“Lissu
ameshapata huruma kubwa ya wananchi. Matusi mengi anayotukanwa yanamjenga.
Tumesikia Spika akisema watakatisha mshahara wake, huko nako ni kumjenga maana
watu wanajadili mshahara huo. Yaani hatapata tabu kupigiwa kura kwa kuwa
ameshajijenga wakati huu,”
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dodoma Dk Paul Luisulie alipata kueleza kuwa mpaka sasa
athari za ziara ya Lissu zimeshaanza kuonekana, kwa kuwa mjadala ni mkubwa.
Ndani ya CCM kwenyewe wanajadiliana na wa wapinzani pia kuna mjadala. Hiyo ni
impact.
“Kwa
upande wa CCM tunajua Rais Magufuli yupo, lakini kwa upinzani Lissu alishasema
atagombea, Hata kama hawakuwa na mpango wa kumpitisha, lazima atakuwa na ushawishi
mkubwa.”
Ujasiri
wa Lissu unapaswa kuwa chachu kwa vijana ambao wanaamini harakati zake ni faida
kubwa kwao kama atachaguliwa.
Baadhi
ya wanachama wa vyama vya upinzni kwa nyakati tofauti, wameliambia RAI kuwa kwa
sasa Lissu ndio nembo halisi ya upinzani
nchini hivyo anapaswa kupewa jukumu la kupeperusha bendera ya urais kwenye
uchaguzi Mkuu ujao.
The post Lissu arudi ‘kitandani’ appeared first on Gazeti la Rai.
↧